Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imefanya ziara katika Vyuo Zanzibar ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa utaratibu wake wa kuhamasisha na kuelimisha wanafunzi wa Vyuo mbalimbali nchini kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma.
Ziara hiyo ambayo ilifanyika kwa ushirikiano kati ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Zanzibar ililenga kutoa hamasa na elimu kwa wanafunzi wa Vyuo kama sehemu ya wadau katika mchakato wa Ajira.
Katika ziara hiyo mada mbalimbali zimeweza kutolewa kwa wanafunzi hao ikiwemo taratibu za uendeshaji wa Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma na changamoto zake, Masharti ya msingi ya kuzingatiwa kabla na baada ya kuwasilisha maombi ya kazi, Matumizi ya TEHAMA hususani namna ya kujisajili katika mfumo wa maombi ya kazi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira Bibi Riziki Abraham akiongea na wanafunzi wa Vyuo mbalimbali alibainisha kuwa mada hizo zimelenga kutoa uelewa kwa wanafunzi wa Vyuo ili waweze kujua majukumu ya Sekretarieti ya Ajira, taratibu za kufuata kabla ya kuomba ajira Serikalini, namna ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili pamoja na utaratibu wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao ujulikanao kama Recruitment portal.
“Wanafunzi wa vyuo kama sehemu ya wadau wetu wakubwa katika masuala ya ajira ni mategemeo yetu kuwa mtakapohitimu masomo yenu mtaingia kwenye soko la ajira, hivyo ni vizuri mkafahamu taratibu za kuomba kazi, namna ya kuandaa wasifu binafsi (CV) namna ya kuandika barua za maombi ya kazi, jinsi ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili na utaratibu mpya wa utumaji na upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya Mtandao ujulikanao kama Recruitment portal” ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kushindana katika soko la ajira nchini, alisisitiza Riziki.
Vyuo Vikuu vilivyotembelewa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Zanzibar, Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar pamoja na Chuo Kikuu cha Sumait.
Aidha, ziara hiyo pia ililenga kutoa uelewa kwa wanafunzi wa Vyuo kuzifahamu Wizara na Taasisi zinazotekeleza masuala ya Muungano ambapo katika mchakato wa Ajira kwa Wizara na Taasisi hizo waombaji kazi kutoka Tanzania Bara wanapata asilimia 79 na waombaji kazi kutoka Zanzibar asilimia 21 ya mgao wa Ajira kwenye Wizara na Taasisi hizo za Muungano.
Mkurugenzi wa Mipango na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Bw. Hamis Haji Juma wakati akizungumza na wanafunzi wa vyuo hivyo alibainisha kuwa ziara hiyo imesaidia kuwaelimisha wanafunzi kujua fursa za Ajira kwa upana wake ikiwa ni pamoja na waombaji kazi kutoka Zanzibar kuomba nafasi za kazi zinatotangazwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ajira zinazotangazwa kupitia Wizara na Taasisi zenye masuala ya Muungano.
Ziara hiyo pia imetumika kuwafahamisha wadau mbalimbali ikiwemo wanafunzi wa Vyuo hivyo juu ya uwepo wa Ofisi ya Sekretarieti ya Ajira katika eneo la Shangani Zanzibar ambayo itasaidia kuboresha utendaji kazi na kuratibu masuala mtambuka yanayohusiana na uendeshaji wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma hasa katika Wizara na Taasisi za Muungano.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment