JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu : +255-22-2114512, 2116898
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Mei, 2017 amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela iliyopo katika hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwashukuru Madaktari na Wauguzi kwa juhudi kubwa wanazofanya kunusuru maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamewatembelea wagonjwa hao majira ya saa moja ya asubuhi wakitokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambako wamehudhuria ibada ya Jumapili.
Miongoni mwa wagonjwa waliojuliwa hali na Mhe. Rais Magufuli na mkewe ni Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) aliyelazwa katika chumba namba 310 na Mtoto Shukuru Musa Kisonga aliyelazwa katika chumba namba 312 ambaye hivi karibuni aliripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika uliosababisha aishi kwa kunywa mafuta ya kula, sukari na Maziwa.
Pamoja na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela na kuwashukuru Madaktari na Wauguzi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo na changamoto zinazowakabili madaktari na wauguzi.
“Jamani, Madaktari tunawashukuru sana, mnafanya kazi nzuri, Madaktari
wote nchini pokeeni pongezi zangu, sisi Serikali tutaendelea kuzikabili
changamoto hizo na siku moja zitakwisha, kikubwa ni kumtanguliza Mungu
mnapofanya kazi ya kuokoa maisha ya watu kwa juhudi kubwa, mnafanya kazi
ya Mungu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
Prof. Lawrence Museru amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwatembelea
wagonjwa katika hospitali hiyo na amemhakikishia kuwa Madaktari tayari
wamegundua magonjwa yanayowakabili Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) na Mtoto Shukuru Musa Kisonga na kwamba wanaendelea vizuri na matibabu.
Aidha, Prof. Museru amesema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa ya
kujenga uwezo wa kutibu magonjwa ambayo wagonjwa walilazimika kwenda
kutibiwa nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha nyingi za Serikali.
“Mhe. Rais hospitali yetu sasa imeanza kufanya upasuaji na kutoa tiba
ya magonjwa ambayo yalilazimu wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi,
mfano hivi sasa tunatoa huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa takribani
250, na kuanzia mwezi Julai mwaka huu tutaanza kupandikiza figo.
“Huduma hii hugharimu kati ya Shilingi Milioni 60 na Shilingi Milioni
70 kwa mgonjwa mmoja anayekwenda kutibiwa nje ya nchi, lakini hapa
nchini gharama zinashuka hadi Shilingi Milioni 21” amesema Prof. Museru.
Prof. Museru ameongeza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili pia
inajipanga kuanza kutoa huduma ya matibabu kwa watoto wenye matatizo ya
usikivu ambao wapo hatarini kuwa viziwi na hivyo kuokoa fedha nyingi
zinazotumika kuwatibu nje ya nchi, kutoka Shilingi Milioni 90 hadi
Shilingi Milioni 30.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Mei, 2017
No comments:
Post a Comment