Serikali imeamua kumchukua mzee ambaye inasemekana ndiye aliyebuni nembo ya Taifa hayo yamethibitishwa na naibu waziri wa afya Dr.Kigwangala kupitia mtandao wake wa facebook nakuandika maneno yafuatayo
Leo asubuhi nilifuatilia matibabu ya Mzee Francis Maige Ngosha (aliyebuni Nembo ya Taifa). Anasema alishirikiana na Ndg. Ali Panga Mazanga kwenye kazi hiyo. Mwenzake ni marehemu kwa sasa.
Hali yake ni dhoofu sana na anahitaji huduma ya Karibu ya wataalamu. Nimemhamishia Muhimbili National Hospital ambako anafanyiwa uchunguzi wa kina. Baada ya kupata ufumbuzi wa tatizo la #afya yake, tutakuwa tumejipanga juu ya namna ya kumhudumia kwenye mambo mengine ya maisha yake.
Itoshe kusema kuwa, Mzee huyu, kama ilivyo kwa wazee wengine, ana haki ya kupata huduma zote za kibinadamu zenye staha sawa na wanadamu wengine. Serikali inaahidi kumhudumia. Wazee kama Ndg. Francis Ngosha walijitoa sana enzi za ujana wao kwa uzalendo na mapenzi ya dhati kwa nchi yetu, walitumia elimu, ujuzi, vipaji na ubunifu wa hali ya juu kutoa mchango kwenye ujenzi wa Taifa tunalofaidi leo, mara nyingi walifanya hivyo bila kujali wao wenyewe binafsi wanapata nini. Na walijisikia raha na faraja kubwa kupata fursa ya kutoa mchango kwenye ujenzi wa nchi yao. Mungu atujaaliye na sisi wa leo tupate walau nusu tu ya mapenzi ya namna hii kwa nchi yetu.
Sisi wa leo tuna jukumu la kuwalinda na kuwaenzi wazee hawa. Nimejisikia faraja na heshima kubwa sana kupata fursa ya kumhudumia walau huyu mmoja. #HK #Dr_Kigwangalla #HamisiKigwangalla #MzeeWaField #SiasaNiVitendo #Uzalendo
No comments:
Post a Comment