WAYNE Rooney ni kiumbe mvumilivu sana. Unamwona jinsi anavyocheza siku hizi? Haleti matumaini kama ilivyokuwa zamani. Amevumilia sana kubaki mchezoni akidhani kiwango chake kitarudi tena. Amechelewa.
Ni kama vile mtu anayetumia simu inayokaribia kuisha chaji angali akijua umeme hakuna, atacheza ‘gemu’ la nyoka akijua umeme utarudi muda si mrefu. Huyu anasikitisha.
Rooney anasikitisha ukimwona anavyocheza siku hizi na pia amechelewa sana kustaafu. Hivi sasa anajichosha tu.
Achana na yote hayo, mpaka jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu England, Rooney bado alikuwa akiheshimika kama nahodha wa Man United. Jose Mourinho analijua, Sir Bobby Charlton analijua hilo.
Kile kitambaa amekivaa tangu 2014, hebu sasa awapishe na wenzake wafaidi heshima ya kitambaa cha unahodha.
Na wenzake hao ni wale ambao walipata nafasi chache za kukivaa, sasa United ni wazi itahitaji nahodha wa muda mrefu kwa ajili ya msimu ujao.
Ni nahodha msaidizi Michael Carrick ambaye atakichukua jumla au Chris Smalling? Hawa hapa nyota watano wa United ambao wana uwezo mzuri wa kuiongoza timu hiyo wakiwa na kitambaa hicho cha heshima.
Ander Herrera
Ni mchezaji gani mwingine anayependwa na mashabiki wa United msimu huu zaidi ya kiungo huyo mahiri kutoka Hispania?
Huu ni msimu bora kwa Herrera. Amecheza soka akiwa na furaha moyoni. Furaha inayochangiwa na kuvaa jezi ya timu aliyokuwa akiiota utotoni.
Kudhihirisha kuwa huu ni msimu bora kwa Herrera, tuzo ya mchezaji bora wa mwaka United inayopigiwa kura na wachezaji wenyewe, alikabidhiwa yeye na kuwapiku watu kama Antonio Valencia, David de Gea na Zlatan Ibrahimovic.
Anastahili kiujumla. Hata ukimuuliza mdau wa United, ni mchezaji gani aliyevaa jezi ya klabu hiyo na kucheza kwa moyo wake wote licha ya changamoto za hapa na pale, atakutajia Herrera.
Lakini kwa upande wake, Herrera bado hajajiamini kama anastahili kuwa nahodha, bado anataka kushinda taji na United, ni nini kitakachofanikisha yote hayo? Upambanaji wake maradufu.
Antonio Valencia
Valencia ameonesha uwezo wa hali ya juu kwenye mbavu ya kulia msimu huu.
Ni mmoja wa wachezaji wanaopendwa sana pale United na mashabiki huenda wakafurahi zaidi kama atapewa kitambaa cha unahodha, kutokana na mchango wake ndani ya timu hiyo tangu 2009, akicheza mechi zaidi ya 200.
Achana na mashabiki. Kuna mtu mwingine anayemkubali sana Valencia pale United, si mwingine ni Mourinho.
Mourinho aliwahi kusema msimu huu kuwa Valencia ni beki bora wa kulia duniani.
Kwa taarifa yako; Valencia atavaa kitambaa cha unahodha kwenye fainali ya Ligi ya Europa keshokutwa dhidi ya Ajax. Ni dalili njema kwa Valencia?
David de Gea
Njia pekee itakayofanikisha David de Gea avae kitambaa cha unahodha msimu ujao ni hii; atangaze wazi kuwa anabaki United, alitupilie mbali dili la kuhamia Real Madrid halafu akubali kumwaga wino kwenye mkataba mpya wa muda mrefu.
Hivyo tu.
Labda inaonekana ni kazi ngumu kumbakisha United, lakini Mourinho anaamini atabaki.
Ukiwazungumzia walinda milango bora duniani, huwezi kuliacha jina la de Gea. Tangu 2011 alipotua Old Trafford akitokea Atletico Madrid, de Gea amejihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwa uwezo wake wa kuokoa michomo mikali licha ya klabu hiyo kukumbwa na changamoto mbalimbali.
Kitakachofanikisha kumwona de Gea akiwa nahodha wa United, ni saini tu kwenye mkataba mpya na si kingine.
No comments:
Post a Comment