Klabu
ya wekundu wa msimbazi , Simba imefanikiwa kunasa saini ya kipa bora wa
ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2016/2017 aliyekua akiichezea Azam FC,
Aishi Manula .
Aishi Manula ambaye amejifunga kwa miaka miwili Simba , anamfuata
aliyekua nahodha wake , John Bocco ambaye tayari ameshatia saini
kuwatumikia wekundu wa msimbazi kwa msimu ujao .
Taarifa za ndani kutoka klabu ya Azam FC zinasema kuwa klabu hiyo
kwasasa ina mpango wa kubana matumizi huku ikigoma kutoa pesa za
kuwasajili wachezaji wake wanaomaliza mikataba. Ukiachana na Bocco na
Manula , huenda Azam FC ikawapoteza nyota wake muhimu zaidi ya saba .
Simba imempata Manula wakati ambao anashikilia rekodi ya kuwa kipa pekee
aliyeweza kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara na kisha
kuitetea. Kipa huyo aliyeibuliwa na Azam amekubali mkataba wa Sh50
milioni kujiunga na Simba na kuitosa Singida United iliyokuwa imempatia
ofa ya Sh60 milioni.
Sababu kubwa za Manula kuacha fedha ndefu ya Singida na kutua Simba
imetajwa kuwa ni timu hiyo kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani
pamoja na mapenzi yake ya kuendelea kusalia jijini Dar es Salaam kufanya
shughuli zake nyingine. Simba itacheza Kombe la Shirikisho.
Manula amekuwa katika kiwango cha juu katika kipindi cha miaka minne
sasa ambapo mbali na kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu mara mbili
(2016 na 2017), alikuwa kipa namba mbili Kombe la Kagame mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment