Mlinda mlango wa Azam FC na timu ya taifa ya Tanzania Aishi Salum Manula, amekanusha kusaini na Klabu ya Simba huku akiongeza kuwa vipo vilabu vingi vya hapa nchini alivyofanya navyo mazungumzo na muda ukifika itajulikana na timu gani ataitumikia.
Aishi amekiri kuwa sasa yeye bado ni mlinda mlango wa Azam FC lakini ameshafanya nao mazungumzo na wamekubaliana kuondoka mkataba wake utakapoisha huku akiongeza ya kuwa amepata ofa nyingi za vilabu vya ndani lakini kwa sasa bado sio muda mwafaka wa kutaja klabu atakayojiunga nayo baada ya kumalizana na Azam FC.
“Cha kusema kuhusiana na suala la mimi kutoka Azam FC ilo niwahakikishie mashabiki na wapenda Soka Watanzania kwamba ni kweli mkataba wangu utakapoisha Azam FC nitaondoka ndani ya Azam lakini kuhusiana na ofa ni kweli kuna ofa nyingi nimepata ndani ya nchi na tuliweza kuzungumza na hizo klabu ambazo zinanihitaji na mazungumzo yameenda vizuri na yanaendelea vizuri kwa ujumla” amesema Aishi Manula.
Aishi amekanusha yeye kusaini mkataba na klabu ya Simba
“Mimi sijasaini Simba na nasikia kuna mkataba unaonyesha kwamba nimesaini Simba, hizo nadhani ni watu wanajitahidi kutaka kujua au kuwathibitishia mashabiki waamini kwamba nimesaini Simba lakini sio kweli, na kama ningekuwa nimesaini Simba nadhani wao wenyewe wangeshanitangaza, ” amesema Aishi Manula.
Aishi amesisitiza kuwa mpaka sasa bado hajajiunga na klabu yoyote hapa nchini huku akiwataka mashabiki kuwa tayari kwani muda utakapofika ataweka wazi kila kitu.
“Kuhusiana na kujiunga na klabu yoyote hapa nchini bado na sio muda mwafaka wa mimi kutaja Klabu ambayo nitaenda kujiunga nayo lakini wakae tayari wakinisubiri mkataba wangu utakapoisha Julai mwaka huu ndani ya Azam FC nitaweka wazi wapi naenda lakini kuhusiana na mkataba sio kweli na sijasaini na timu yoyote” amesema Aishi Manula
No comments:
Post a Comment