Breaking

PAKUA MCHAINA APP HAPA CHINI USOME HABARI ZETU HATA USIPOKUWA NA MB

Wednesday, September 13, 2017

MAMIA WAGOMBEA NAFASI ZA KAZI 45 KIBITI LICHA YA WILAYA HIYO KUOGOPWA



AMA kweli tatizo la ajira ni kubwa! Mamia ya watu wamejitokeza kuwania nafasi 45 tu za ajira zilizotangazwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.






Idadi hiyo kubwa ya waombaji, imewashangaza hadi viongozi wa wilaya hiyo ambayo hivi karibuni ilikumbwa na misukosuko mikubwa ya kiusalama, hasa baada ya kuwapo kwa taarifa za kila mara za kuuawa kwa watendaji na wananchi wasio na hatia kulikotokana na ’unyama’ uliokuwa ukitekelezwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwamo Jeshi la Polisi, vilichukua hatua kadhaa za kurejesha utulivu wilayani humo na sasa, mamia ya watu wamejitokeza kuchangamkia fursa za ajira zilizotangazwa wilayani humo mwishoni mwa mwezi uliopita.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Alvera Ndabagoye, alisema tofauti na matarajio yao, mamia ya watu ambao idadi yao kamili bado inaratibiwa wamejitokeza ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kutoka kwa tangazo lao mwezi uliopita.

“Watu waliojitokeza ni wengi… idadi yao tutaitoa baada ya kumaliza kurekodi,” alisema Ndabagoye.

Awali, Mkurugenzi huyo alisema waombaji watakwenda kujaza nafasi za kazi 45 kwenye halmashauri hiyo.

Maofisa watendaji wa vijiji ni miongoni mwa nafasi hizo zinazowaniwa baada ya baadhi yao kukosekana kwa sasa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya kufariki dunia na pia kuziba mapengo ya watumishi walioondolewa kwa kukosa sifa. Mwisho wa kutuma maombi kwa kila nafasi ilikuwa juzi.

Hivi karibuni, watu 56,000 walijitokeza kuomba kazi katika nafasi 400 zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), huku 30,000 kati yao wakibahatika kuitwa katika usaili.

Aidha, Kibiti ni miongoni mwa wilaya nne za mkoa wa Pwani zilizoundiwa mkoa maalumu wa Kipolisi hivi karibuni kutokana na changamoto za kiusalama zilizokuwapo, nyingine zikiwa ni Rufiji, Mkuranga na Mafia.

Kuanzia mwaka jana, maeneo hayo yalikuwa yakikabiliwa na mauaji ya viongozi wa ngazi mbalimbali na pia raia wasio na hatia, ambayo yalikuwa yakitekelezwa na watu wasiofahamika huku mara nyingi yakihusisha uvamizi kwenye nyumba za wahusika na pia matumizi ya risasi. Kutokana na kushamiri kwa mauaji hayo na vitisho vilivyokuwa vikitolewa na wauaji, baadhi ya watendaji walilazimika kukimbia makazi yao.

Tukio la mwisho kutokea wilayani Kibiti ni la Juni 27, ambapo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangwi, Michael icholaus na mtendaji wa kijiji hicho kilichoko Kata ya Mchukwi, Mwilami Shamte, waliuawa kwa kupigwa risasi na kufanya idadi ya waliokwishauawa Pwani kufikia 37.

Hali ya kurejesha amani wilayani humo ilitokana na juhudi za jeshi la polisi nchini, chini ya IGP Simon Sirro, ambaye mara baada ya kuteuliwa alifanikiwa kukomesha mauaji hayo na polisi ilitangaza kuwaua watuhumiwa wa mauaji 13 waliodaiwa kutekeleza mauaji Kibiti, Mkuranga na Rufiji. 


CREDIT:YUVINUSM.CO.TZ