BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)
TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU WAHITIMU WA STASHAHADA KATIKA PROGRAMU MBALIMBALI
WANAOKUSUDIA KUOMBA KUJIENDELEZA KATIKA NGAZI YA SHAHADA KATIKA VYUO VYA
ELIMU YA JUU KWA MWAKA WA MASOMO 2017/2018
Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa Sheria
ya Bunge, Sura 129, ili kusimamia na kuratibu utoaji wa mafunzo ya elimu
ya ufundi nchini. Jukumu kubwa la Baraza ni kuendeleza na kuinua ubora
wa elimu na mafunzo ya ufundi nchini kwa kusimamia kikamilifu shughuli
za usajili na ithibati, mitaala na upimaji ili tuzo zitolewazo na
vyuo/taasisi ziwe na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa. Kifungu
cha 5 (1) (e) na (f) cha Sheria hii kinaipa mamlaka NACTE, kuanzisha
tuzo mbalimbali zinazotolewa na kuhakikisha kuwa ubora wa elimu na
mafunzo ya kada ya kati yatolewayo na taasisi mbalimbali yanazingatia
ubora unaokusudiwa. Aidha, Kifungu cha 11, kinalitaka Baraza kuhakikisha
kuwa Tuzo zitolewazo na vyuo na taasisi zote zinazoendesha mafunzo ya
kada ya kati zinatambuliwa na mamlaka husika. Katika muktadha huu, kila
chuo/taasisi inayotoa elimu ya ufundi inatakiwa kuwasilisha Baraza
matokeo ya mitihani kila mwisho wa semista.
Ili
kulifanikisha hili, Baraza limeandaa mfumo ambao taasisi/chuo kitapata
taarifa za muombaji mwenye sifa linganifu (muhitimu wa Stashahada) moja
kwa moja.
Hivyo,
wahitimu wote wa Stashahada yoyote wanaokusudia kuomba kujiendeleza
katika ngazi ya Shahada wanatakiwa kuhakiki taarifa zao Baraza (NACTE)
kabla ya kufanya maombi yao kwenye taasisi/vyuo wanavyotaka kwenda
kusoma. Uhakiki huo utafanywa kwa njia ya mtandao (online) kupitia Mfumo wa Uhakiki wa Tuzo (NACTE Award Verification System - NAVS) kwa kubofya hapa au kupiti tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz) kwa kubofya kitufe kilicho andikwa Award Verification. Baada ya kuhakiki taarifa zake kuwa kamilifu na sahihi, mhakiki atapatiwa Namba ya Utambulisho (Award Verification Number - AVN)
ambayo itaambatanishwa na maombi ya Udahili kwenye taasisi/chuo husika.
Utambulisho huo utatumiwa na taasisi/chuo kujiridhisha kwamba taarifa
alizowasilisha muombaji wa Udahili ni sahihi na hivyo kuweza kudahiliwa
na kisha kuchaguliwa kwa ajili ya masomo kulingana na mahitaji ya
taasisi/chuo husika.
Aidha, Baraza linapenda pia kuwafahamisha wale wote walio na Stashahada walizopata nje ya nchi (Foreign Diploma Awards), nao waziwasilishe kupitia mfumo huu (NAVS)
kwa ajili ya kuzifanyia ulinganifu na kuweka taarifa zao kwenye
Kanzidata ya Baraza ili nao waweze kupata Namba ya Utambulisho. Maelezo
ya namna ya kuziwasilisha tuzo za kufanyiwa ulinganifu yanapatika kwenye
tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz).
Ili
mwombaji Udahili apate Namba ya Utambulisho atalipa Shilingi Elfu Kumi
(10,000/=) kwa njia ya mtandao (Online) kwa kufuata maelekezo yaliyopo
kwenye Mfumo wa Uhakiki wa Tuzo - NAVS. Kwa wale
wanaotaka kufanya ulinganifu wa vyeti vyao, watatakiwa kulipa Shilingi
Elfu Ishirini (20,000/=) kwa tuzo za ndani ambazo hazisimamiwi na
baraza, na Shilingi Elfu Hamsini (50,000/=) kwa tuzo za nje ya nchi
(foreign awards).
Baraza
linapenda kuwafahamisha wahitimu wa Stashahada wanaotaka kujiendeleza
katika ngazi ya Shahada kuwa wanaweza kufanya uhakiki huo kuanzia leo
tarehe 28 Juni, 2017 hadi tarehe 20 Julai, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)
TAREHE: 28/06/2017
No comments:
Post a Comment