Na Jumia Travel Tanzania
Inastaajabisha
kuona watu wa mataifa ya nje wanajua vitu vingi zaidi vinavyopatikana
Tanzania kuliko watanzania wenyewe. Sijui ni ile hulka ya kutopenda
kufuatilia mambo au ni dhana kwamba waache wageni waje kushangaa maana
hivyo vitu vitaendelea kuwepo tu.
Nchi
yetu imebarikiwa na inaendelea kubarikiwa kugunduliwa kwa mambo mengi
zaidi ya kustaajabisha ambayo hayapatikani kwingineko duniani. Jumia
Travel ingependa kukufumbua macho kwamba yafuatayo ni baadhi tu ya mambo
yanayopatikana na unaweza kuyashuhudia ukiwa nchini Tanzania.
Mti
mrefu zaidi barani Afrika. Hivi karibuni mtafiti kutokea Chuo Kikuu cha
Byreuth cha nchini Ujerumani, Dkt. Andreas Hemp baada ya utafiti wa
takribani miaka 20 amethibitisha kuwa Tanzania ina mti mrefu zaidi
kuliko yote barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 81.5. Mti huo kwa jina
la kitaalamu unajulikana kama ‘Entandrophragmaexcelsum’, ni aina adimu
sana ya miti na inaweza kuwa na umri wa zaidi ya miaka 600. Ili kuweza
kuuona mti huo unaopatikana katika safu ya misitu ya Mlima Kilimanjaro
na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii hivi sasa, itakupasa utembee umbali
wa masaa 2.30 mpaka kutokea kijiji cha Tema ili kuufikia.
Twiga mweupe aonekana kwa mara ya kwanza. kubisha
kwamba hiko kitu hakiwezekani lakini ndio maajabu ya Mungu hayo, twiga
mweupe ameonekana Tanzania. Takribani mwaka mmoja uliopita, mwanzilishi
na mwanasayansi katika Taasisi ya Misitu Asilia katika hifadhi ya taifa
ya Tarangire inayopatikana mkoani Manyara, Dkt. Derek Lee alimuona twiga
mwenye rangi nyeupe. Twiga huyo ambaye alikuwa na umri wa miezi 15
amepewa jina la ‘OMO,’ rangi yake inaonekana kama vile imechubuliwa
tofauti na rangi asilia ya twiga tunaowajua. Mtafiti huyo amesema kuwa
twiga huyo anasumbuliwa na ‘leucism,’ ni hali inayosababisha kupotea kwa
baadhi ya rangi. Licha ya utofauti huo na wenzake lakini bado mnyama
huyo anajichanganya na wengine na wenzie kutojali utofauti huo kabisa.
Asilimia
30% ya ardhi ya Tanzania ni hifadhi za wanyama pori. Kama ulikuwa
haujui basi ni kwamba nchi ya Tanzania sehemu ya asilimia 30 ya ardhi
yake ni hifadhi za wanyama pori wa aina mbalimbali duniani. Tanzania
inazo hifadhi za taifa 16 ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) ambapo kwa ujumla wake zina ukubwa wa kilometa
za mraba takribani 42,000. Kwa mfano, hifadhi ya taifa ya mbuga ya
Serengeti ni mojawapo ya mbuga maarufu na inayopendwa zaidi duniani, ni
makazi ya aina mbalimbali za wanyama zaidi ya milioni moja. Pia
imetangazwa kuwa ni Eneo la Urithi wa Dunia na kutajwa mojawapo ya
sehemu ya Maajabu Saba ya Dunia.
Takribani
wanyama milioni 2 hushiriki tukio la kuhama linalotokea kila mwaka
mbuga ya Serengeti. Kila mwaka watalii hushuhudia tukio la kipekee la
uhamaji wa makundi ya wanyama wa aina ya pundamilia na nyumbu zaidi ya
milioni 1.5. Tukio hilo hutokea kati ya Kusini mwa bonde la mbuga ya
Serengeti nchini Tanzania kuelekea eneo la Kaskazini mwa mbuga ya Masai
Mara iliyopo Kenya. Lengo kubwa la tukio hilo ni katika harakati za
kutafuta malisho mazuri kwa wanyama hao ambalo hutukia mnamo miezi ya
Mei mpaka Desemba ingawa muda huwa unaweza kubadilika. Sehemu
inayosisimua zaidi ni pale wanyama hao wanakatisha mto Mara kuuvuka
kuelekea Masai Mara, wanyama hao kwa makundi na ujasiri mkubwa huvuka
licha ya kuwa na mamba wakali.
Mbuyu
unaweza kuishi mpaka miaka 1,000. Mibuyu ni miti mikubwa na inayovutia
zaidi, hapa nchini Tanzania unaweza kuiona vizuri zaidi ukitembelea
hifadhi ya taifa ya Tarangire. Kama ulikuwa haufahamu ni kwamba baadhi
ya aina ya miti ya mibuyu huweza kuishi kwa takribani miaka 1,000 au
zaidi. Inasemekana mbuyu mkongwe zaidi unapatikana nchini Afrika ya
Kusini ni unaaminika kuwa na miaka takribani 6,000.
Uwepo
wa vitu hivyo Tanzania ni uthibitisho wa namna nchi hii ilivyobarikiwa
na vivutio mbalimbali ambavyo watu wengi hawavifahamu bado. Kwa hayo
machache Jumia Travel inaamini utakuwa umejifunza na kupata shauku ya
kutembelea maeneo hayo pamoja na kukuongezea ari ya kujifunza mengineyo
zaidi.
No comments:
Post a Comment