Ikiwa imepita siku moja tokea kumaliza kutumikia kifungo chake msemaji wa Yanga, Jerry Muro amesema adhabu aliyopewa haikuwa halali dhidi yake huku akidai kikombe alichonywea yeye ndicho wanachonywea wengine nyuma yake.
Murro ambaye alikuwa na kifungo cha kutojihusisha na masuala ya soka kwa kipindi cha mwaka mmoja, hukumu iliyotolewa Julai 2 mwaka 2016, amefunguka zaidi baada ya kufika ukomo wa kifungo chake.
“Nilipewa adhabu ambayo haikuwa sawa na nilikaa kimya kwa sababu sikutaka kushindana na mtu cha msingi tu tulijua tatizo liko wapi na maadui zetu wakoje tukaa kimya sasa adhabu imeisha. Unachomfanyia mtu hapa duniani ujue unalipwa hapa hapa duniani kabla ya kufa, mimi nimekandamizwa, nimeteswa na nimeonewa. Kikombe nilichonywea mimi ndiyo wanachonywea wengine nyuma yangu na wasipotubu pamoja na kuungama mbele za Mungu hii dhambi itawatafuna”, alisema Muro.
Pamoja na hayo, Muro amesema hatma ya yeye kurejea katika nafasi yake ya kuwa msemaji wa klabu kwa sasa amewaachia wanachama ili waweze kuamua kama watamuitaji aendelee kuwatumikia au aachane nao.
“Inapofika suala la mpira wa miguu mimi ni mwanachama na mdau wa Yanga tu sina maamuzi ya aina yeyote ila nawachia wanayanga wenyewe waseme kama watanihitaji na ikitokea wanayanga wakisema hawanitaki kwanini niendelee kupambana nao kwani mimi ni nani”, alisisitiza Muro
Wakati msemaji huyo wa Yanga akimaliza kifungo chake, msemaji mwenzake wa timu ya Simba Haji Manara naye anatumikia adhabu hiyo hiyo ya mwaka mmoja
No comments:
Post a Comment