Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Jamal Malinzi na wenzake wawili akiwemo Katibu Mkuu wake, Mwesigwa Celestine, wamerudishwa rumande hadi tarehe 17 Julai kesi yao itakapotajwa tena.
Hatua hiyo ni baada ya watuhumiwa hao leo kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kesi yao kutajwa, ambapo mawakili wa upande wa utetezi waliwasilisha maombi mawili ambayo ni kuomba dhamana, na kuomba kesi yao ianze kusikilizwa.
Baada ya maombi hayo kusikilizwa ikiwa ni pamoja na hoja kutoka pande zote, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Wilbard Mashauri akatoa maamuzi ya kuyakataa maombi yote mawili, na kuamuru washtakiwa hao warudishwe rumande.
Hakimu Mashauri pia amewapiga marufuku mawakili wa upande wa utetezi kuacha kuzungumzia kesi hiyo kwenye vyombo vya habari kwa lengo la kupata huruma ya wananchi, na kuwataka kufuata sheria.
Amewaelekeza kuwa wanachopaswa kuzungumza ni kile tu ambacho kimeamuliwa na mahakama, na kuwakumbusha kuwa hata wao hawako juu ya sheria.
Malinzi na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 29, mwaka huu wakikabiliwa na mshtaka 28 yakiwemo ya rushwa, utakatishaji fedha na kughushi nyaraka.
No comments:
Post a Comment